ULAJI WA KITIMOTO NI HATARI SANAA KWA AFYA YA BINADAMU
Dar es Salaam. Hatari! Watu wanaokula nyama ya nguruwe ambayo itakuwa haijaivishwa vizuri wako katika hatari ya kuambukizwa minyoo aina ya tegu na magonjwa mbalimbali ukiwamo wa kifafa.
Hayo ni matokeo ya utafiti uliofanywa na wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) hivi karibuni katika wilaya za Mbulu, Kongwa, Sumbawanga, Mpanda, Iringa, Urambo na Mbozi ambako walibaini kuwa ulaji wa nyama hiyo maarufu kama kitimoto ni hatari zaidi kwa afya ya binadamu.
Kiongozi wa jopo la watafiti hao, Mhadhiri wa UDSM, Chacha Mwita alisema kati ya watu 1,036 waliofanyiwa vipimo, 150 walikutwa na maambukizi ya minyoo hiyo na kwamba walibaini kuwepo kwa mzunguko mkubwa wa minyoo ya tegu baina ya nguruwe na binadamu jambo ambalo ni hatari kiafya.
Kwa mujibu wa utafiti huo uliopewa jina la “Tegu wa Nguruwe na Binadamu”, asilimia 53 ya wagonjwa wa kifafa nchini wametokana na ulaji wa nyama hiyo.
“Kati ya hao 150 waliokutwa na maambukizi hayo, zaidi ya 20 walikuwa na ugonjwa wa kifafa huku asilimia 53 wakiwa wamesababishiwa na minyoo ya tegu,” alisema Mwita katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi jana.
Mtafiti huyo alisema japokuwa Serikali haijaweka kipaumbele katika kudhibiti magonjwa yanayoambukizwa na wanyama, ipo haja ya kupata vipimo vinavyoweza kutambua maambukizi ya wadudu hao kwa binadamu wanapoingia kwenye damu na kuweka makazi kwenye ubongo, moyo, macho na maeneo mengine ili iwe rahisi kudhibiti.
Kinachotokea
Dk Mwita alisema awali, binadamu ndiye ambaye huwa wa kwanza kumwambukiza nguruwe minyoo ya tegu. Minyoo ikiwa kwenye tumbo la binadamu, kwa hatua ya kwanza huwa na pingili ambazo zikiwa na mayai hukatika na kutoka binadamu anapojisaidia.
Katika pingili moja, hukaa mayai yapatayo milioni moja na kwamba baada ya kutoka kwa njia ya kinyesi hupasuka na ikiwa nguruwe atakula mayai hayo kutoka kwenye kinyesi, huingia kwenye mfumo wa damu na kujikita kwenye nyama kisha huanguliwa na kuendelea kuzaliana kwa kasi wakati huo wakiwa kwenye muundo mwingine.
“Wilaya ya Mbulu ilikuwa hatari zaidi kwa sababu kila nguruwe tuliyemfanyia utafiti tulikutana na minyoo mingi, huku idadi kubwa ya watu wakiwa wameambukizwa,” alisema Mwita.
Mtafiti huyo alisema sababu ya maambukizi hayo kuwa kubwa ni tabia ya wakazi wa maeneo hayo kutotumia vyoo huku wanyama hao wakiachwa kuzurura ovyo. Hivyo, ikiwa binadamu atakula nyama yenye maambukizi, wadudu hao ambao tayari huwa kwenye muundo mwingine hujikita kwenye kingo za utumbo kisha kuingia kwenye damu na kuanza kutembea na ikifika kwenye ubongo, binadamu huyo huwa kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kifafa.
“Wale wadudu wakikaa kwenye ubongo hujigeuza na kuwa wagumu, hapo husababisha mgandamizo kwenye ubongo na baadaye mtu hupata kifafa,” alisema.
Pia, alisema ikiwa itakimbilia kwenye macho, mlaji huweza kupata upofu na kwamba, mgonjwa huweza kupona ikiwa atagundulika mapema.
Hatua za utafiti
Wakishirikiana na madaktari wa Hospitali ya Wilaya Mbulu, walipata sampuli za damu kwa ajili ya utafiti. Baada ya hapo walikwenda kuifanyia utafiti wao chuoni na kuwabaini waliopata maambukizi ya kifafa.
Mwita alisema watu waliobainika kupata maambukizi ya kifafa walipelekwa Hospitali ya Misheni ya Haydom iliyopo Manyara kufanyiwa vipimo vya ubongo kwa kutumia mashine ya CT-Scan).
Wataalamu wengine walonga
Daktari wa ubongo, kutoka Hospitali ya Hydom, Mshindo Kilawa alisisitiza kwamba ulaji wa kitimoto ni hatari kwa binadamu ikiwa nyama haitaivishwa ipasavyo.
“Tatizo hilo kitaalamu linaitwa ‘Neurocysticercosis’ na husababishwa na minyoo inayoitwa taenia solium,” alieleza.
Comments
Post a Comment