DINI YA KISHETANI YA VUTA WATANZANIA WENGI

Makundi ya dini za waabudu shetani sasa yameamua kujiweka wazi na kutangaza hadharani jinsi ya kumuabudu shetani, hilo halina ubishi tena.
Matangazo kwenye mitandao ya kijamii inawaalika watu kujiunga na kuwapa mbinu za kuwa waabudu shetani.
Uchunguzi wa chanzo cha blog umebaini kuwa, baada ya aliyekuwa kiongozi wa dini hiyo, katika Wilaya ya kimasonary ya Africa Mashariki, Andy Chande, kuendesha mahojiano maalumu, katika kituo kimoja cha radio na kulipamba kundi la Freemason akidai ni chama cha hiari, mamia ya watanzania hasa vijana, wamekuwa wakihaha kujiunga na dini hiyo kwa kasi kubwa.

Wakati Chande akidai kundi hilo sio la kidini, bali ni chama cha hiari mahojiano hayo yanatofautina sana na maelezo ya kina kuhusu kundi hilo, katika kitabu chake kiitwacho Shujaa katika Africa, Safari toka Bukene.

Kwenye Uk. 169, wa kitabu hicho Chande anaeleza mwenyewe kuwa, miongoni mwa digree nyingi alizonazo kulingana na mafunzo aliyoyapata ndani ya kundi hilo, yakiwemo ya matambiko,  sasa yeye ni shujaa namba moja katika mashujaa wa msalaba wa Babeli.

Uchunguzi huo umebaini kuwa, waliotekwa zaidi na matangazo hayo ni makundi ya vijana wa sekondari, wanachuo na watu wa umri wa kati, ambao wanavutwa na tamaa ya kupata utajiri wa haraka haraka.
Baadhi ya vijana kadhaa wamekuwa wakihangaika na kuwatafuta wale wanaoandika makala za mienendo ya makundi haya, wakidai eti wanasaka mbinu za kujiunga.

Jambo la kustaajabisha ni kuwa, vijana wawili walieleza utayatari wa kuwatoa hata wazazi wao kafara ilimradi wapate fedha.

Mmoja wao mwenye umri wa miaka 23, alisema: “Nikipata nafasi ya kujiunga nipo tayari kumtoa yeyote anayehitajika, hata mama kwani siku moja atakufa tu, wacha nile maisha.”

Hiyo ndiyo hali ya kizazi hiki kilichopotoka, ambacho kinawindwa na mawakala wa baba yao ibilisi, ili waende pamoja motoni.

Katika moja ya maelezo kwenye mitandao inayowahamasisha watu kujiunga na kundi hilo kuna maelezo yafuatayo:  Kuna idadi kubwa ya watu waliohitaji kufahamu Freemasons ni nini, baada ya taarifa kuenea kwamba Freemasons, ni dini ya kishetani na watu wengi maarufu wamo humo wakiwemo viongozi wa nchi na mastaa wengine kama;  Jay Z, Rihanna, Beyonce, Kanye West, Celine Dion na hata hapa Tanzania. Juni 2012 magazeti ya udaku yaliwataja wasanii kama Diamond Platnums na Jackline Wolper kwamba wamo humo,  lakini wasanii wenyewe walikanusha.”

Ni katika kuusaka ukweli,  Clouds TV/Radio kupitia kwa mtangazaji  wake Gerald Hando, ilimwalika na kufanya mahojiano na Sir Andy Chande, ambae aliwahi kuwa kiongozi mkuu wa Freemasons Afrika Mashariki, kwenye nchi za Tanzania, Uganda, Kenya na Seychelles.

Katika mahojiano hayo, yanayotajwa kuwa chanzo cha idadi kubwa ya watu kumiminika  katika ibada hiyo, huku wengine wakivamia makao makuu ya Freemasons yaliyopo mkabala na Hoteli ya Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.

Chande alianza kwa kueleza alikotokea akisema; alifika Tanzania mwaka 1950, alihamia Dar es salaam mwaka 1953 na kukutana na watu wengi wa bandarini, Shirika la Reli na mashirika mbalimbali aliyofanyia kazi na alikutana na watu wengi ambao walikuwa wanahudhuria vikao vya Freemasons, akaanza kuuliza ulizia na akajifunza mambo kadhaa kuhusu hao watu.

Kwa wakati huo, hao watu hawakua huru kuzungumzia Freemasons kama anavyofanya Chande sasa hivi, haswa kabla ya vita ya pili ya dunia.

Sir  Chande anasema; wakati huo Freemasons ilikua imegawanywa kwenye makundi tofauti, katika mahospitali, shule, na mashirika mbalimbali na kulikua na kundi maalum la Freemasons kwa ajili ya matajiri na wafanyakazi wakubwa wa serikali, ukiangalia vizuri wengi wao walikua wazungu na baadhi ya wahindi.

Kundi la kwanza lilikua linaongozwa na watu wa Scotland, makundi mawili yaliyofuata yalikua yanaongozwa na waingereza na kundi la nne lilikua linaongozwa na wahindi, ambalo ndilo Chande alilojiunga nalo, ilimchukua miaka miwili kukubaliwa kujiunga na Freemasons, aliapishwa rasmi mwaka 1954 akiwa na umri wa miaka 28, kumbuka kwamba masharti ya kujiunga ni lazima uwe na umri kuanzia miaka 21.
Baada ya hapo ndipo alipoanza kupenda Freemasons ambapo pia alipanda cheo na kupewa nafasi ya kuongoza kundi au tawi la Freemasons katika nchi nne ambazo miongoni mwao ni  Kenya, Tanzania, na Uganda na akajiunga na miradi tofauti ya Freemasons nchini Uingereza yakiwemo mahoteli ya kifahari pamoja na kupewa jukumu la kujenga hoteli mpya ya Freemasons nchini Ghana kwenye mji wa Khumasi ambayo ni ya kifahari sana.Hoteli nyingine ya kifahari alisimamia ujenzi wake iko Zambia.

Mwaka 2005, Sir Andy Chande alistaafu kuwa kiongozi wa Freemasons Afrika Mashariki, baada ya kutumika kwa miaka 19, kwa sasa haudhurii mikutano ya nchi za Afrika Mashariki,  lakini anahudhuria mikutano ya Uingireza kwa sababu bado anafanya kazi na baadhi ya mashirika Uingereza.

FREEMASONS NI NINI?
Kulingana na maelezo ya Chande,  hii ni taasisi iliyoanzishwa miaka 350 iliyopita katika njia ambayo haikua rasmi, ilihalalishwa miaka 300 iliyopita, hatujui vizuri ilianzishwa vipi ila inaaminika walikua wajenzi wanaojenga mashule, makanisa, wakati ule kukiwa hakuna miji mikubwa kama sasa wala mahoteli, na wao walikuwa wakiishi pamoja na familia zao na wakihama wanahama pamoja, wakaanzisha miradi ya kujenga hoteli ndogo ndogo ili kusaidiana kama wajenzi na kujikwamua kiuchumi, wakawa wanafundishana.. yani kama una ujuzi unamsaidia na mwenzako kujua.

Anasema: “Freemasons sio dini na tukikuta wewe ni mkristo tunakushinikiza ukristo wako, kama wewe ni mhindu unabaki kuwa mhindu, lakini Freemasons orijino ilianzishwa na wakristo nchini Uingereza na baadae ikahamia Ulaya, Marekani, Australia na India Freemasons ikaja kuwa kubwa sana.”

Kwa nchi za Afrika Freemasons imekuja kuwa kubwa kwenye nchi kama za Nigeria na Ghana pia Sierra Leone, kwanza aliyewahi kuwa rais wa nchi hiyo Daudi Jawala alikua mmoja wao.

Duniani kote sasa hivi kuna wanachama milioni tatu laki tano wa Freemasons na wanachangia dola za kimarekani zaidi ya milioni 400 kwa ajili ya misaada kila mwaka, yani kwa siku ni zaidi ya dola milioni moja kusaidia afya, elimu vilevile wajane wa wanachama wa Freemasons wanasaidiwa ambapo pia ukiumwa na ukiwa na shida yeyote kuna msaada wa bure unapatiwa, nakumbuka hata Dk.  Charles Matwali alipoumwa sana, tulimpeleka Uingereza kwa matibabu.

MUNGU ANAYEABUDIWA NA FREEMASON
Ili kujiunga ni lazima uwe na umri wa miaka 21, ni hiari kujiunga na pia uwe unamwamini Mungu haijalishi ni Mungu gani, watu ambao hawamuamini Mungu hawaruhusiwi kuwa Freemasons, na lazima uwe mtu mkweli.

Ni lazima familia yako ikubali pia wewe kujiunga na Freemasons kwa sababu Freemasons hawatokubali kujiunga kwako kukufanye uwe masikini kutokana na kutoa misaada.

Unapotaka kujiunga ni lazima upeleke maombi yako kwa mtu unaemfahamu ambae yuko Freemasons, au kama hujui mtu unaandika barua baada ya hapo utapewa nakala za kusoma na kuelewa na kamati ya kukuruhusu kuingia kwenye Freemasons itakupeleleza wewe na familia yako, na pia watakutembelea nyumbani kuongeana mkeo au mumeo au familia kwa siri.

Inaweza kuchukua mwaka mmoja na nusu au mwaka kuruhusiwa kujiunga na Freemasons baada ya kupeleka maombi, ambapo hapo ni kukubaliwa tu, baada ya hapo ili uwe Freemason kamili kuna vyeo vitatu ambavyo tunaviita degrees ambavyo ni lazima uvikamilishe, jambo ambalo linaweza kuchukua zaidi ya miaka miwili.

                                   UTATA KUHUSU IBADA  YA FREEMASONS
Uchunguzi umebaini pia kuwa, mwanachama anatakiwa kujifunza vitu vingi na kuvihifadhi kichwani;  kama vile; maneno ya kusema wakati wa ibada za Freemasons.

Maelezo haya kutoka kwa mkuu wa kundi hili yanadhihirisha utata wa kiimani wa kundi hili na mpango wake wa siri wa kuwateka wanadamu na kuwatenga na
Mungu wa kweli.

Chande akielezea uanachama wake katika kundi hilo, linaloaminika ni la kishetani alisema:

“Acha nizungumzie Freemasons ya Uingereza ambayo mimi ni mmoja wao, Makao makuu yako London kwenye barabara inayoitwa Great queen street, Mkuu wa Freemasons  Uingereza, ni binamu yake malkia Elizabeth ambae tunamuita Grandmaster. Kazi zote zinazofanyika na Freemasons zinaendeshwa kutoka kule, kwa mfano Mv. Bukoba ilivyozama nilipiga simu kule kuomba msaada wakatuma Pound elfu 10,  ingawa na sisi hapa tuna kitengo chetu cha misaada ambayo kilichangia, maamuzi ya misaada mikubwa yanatoka Uingereza.

Kuna mahoteli ya Freemasons Uingereza, Scotland na Ireland na katika nchi zilizokua za kisovieti zamani, tuna mahoteli dunia nzima ambapo kama upo kwenye Freemasons ya Dar es Salaam, unaweza kuhudhuria vikao kwenye hoteli hizo duniani kote, tunazomiliki ambazo zinatumika pia kama kumbi za mikutano yetu ili mradi uthibitisho kwamba wewe ni mmoja wetu.

Watu wengi huwa wanasema ni taasisi inayofanya mambo yake kwa siri, lakini ukweli ni kwamba siri pekee iliyopo ni jinsi nitakavyokutambua kama wewe ni mmoja wetu, vingine vyote viko wazi na vinapatikana hata kwenye internet na unaweza kwenda kwenye maduka ya vitabu kote Afrika Mashariki, hata Uingereza ukapata nakala zote za Freemasons ikiwemo hata maneno tunayosema tukifanya ibada zetu.

Kwa Afrika Mashariki Makao Makuu ya Freemasons yako Nairobi Kenya, kwa sababu aliyechukua nafasi yangu yuko Nairobi na pia makamu wake yuko Nairobi, Kuna majumba 50 ya Freemasons Afrika Mashariki.

Ingawa makao makuu yako Nairobi, jumba la Dar es Salaam, linajitegemea lenyewe na tunafanya miradi yetu na kusajili watu wetu hapa hapa, hatuingiliwi na ofisi ya Nairobi, maamuzi yetu yanafanyika hapa hapa.”

Katika mahojiano haya unaweza kushangaa jinsi ‘kuhani’ huyu anavyojichanganya, kwanza alisema kundi hili sio dini, lakini anadai kuwa kuna vitabu vyenye maneno ya jinsi  ya kufanya ibada ya Kifreemasons. Hebu jiulize taasisi ambayo sio ya dini inawezaje kufanya ibada tena kuwa na ujumbe wa namna ya kuendesha ibada.?

MAHEKALU YA SIRI FREEMASONS DAR
Chande katika mahojiano haya yanayojenga mashaka makubwa na pengine kudhihirisha kuwa hii ni taasisi ya siri anasema, Dar es Salaam, kuna  masonic lodge nne, lakini inayojulikana wazi ni ile ya posta, hizi zingine ziko wapi, zinafanya nini? Ni hoja ya kujadili.

IBADA YA FREEMASONS NA MAELEZO  HILA KUWANASA WATU
Kuhusu ibada Chande anasema: “Ibada inaanza wakati vikao vinaanza, inahusisha mara nyingi kitu ambacho kinafanana na ibada kanisani, mara nyingi inahusika kumuweka mwananchama mpya kwenye mstari na mtazamo mmoja na aliowakuta, na kwenye ibada huwezi kuvaa unavyotaka, lazima uvae suti na tai isipokua nchi kama India ambao hawavai tai.
Ukiwa mwanachama unapewa maswali ambayo ukiyajibu vizuri kwa muda wako unaweza kupandishwa cheo na inachukua muda kufikia digree ya tatu, tukiwa kwenye vikao, Mwenyekiti anaitwa Master na anao wasaidizi wawili, kwenye ibada Mwenyekiti anakaa Mashariki, msaidizi mmoja ana kaa mbele yake akimtizama na wa pili anakua anasaidia kwa shughuli nzima inayoendelea.

Kuna mwingine ambaye ndio muongozaji wa sala na wakati tukisali, Mungu tunamuita fundi mkuu aliyeumba sayari zote, hiyo inahakikisha kwamba uwe Muislamu au Mkristo tunakwenda sambamba.

Kuna alama ya Compass inayotumika kuonyesha mwelekeo kwa mishale yake, kuna ruler na pembe nne ambavyo ni vitu vinavyotumika kwenye ujenzi ila vinaweza kutumika kufundisha kuhusu maisha, na ndio vinatumika hivyo wala sio kuhusu kitu kingine. Tukifanya ibada zetu au kumkubali mtu kuingia Freemasons, lazima avae pajama au mavazi yanayotumika kulalia usiku, na haruhusiwi kuwa na pesa mfukoni, kuvaa saa au cheni  ishara ya kuwa yeye ni maskini kama alivyozaliwa.

Uchawi, kuabudu shetani na mambo kama hayo watu wanayosema kwamba Freemasons ndio inajihusisha na hivyo vitu, ikiwemo kutoa uhai ndugu, ni waongo, hawana ujuzi wa kutosha, nakumbuka pia Rais Moi aliunda kamati maalum kuchunguza uchawi na waabudu shetani na tuliitwa nikaenda kuwaeleza kwa muda wa karibu saa na nusu kuhusu Freemasons, ingawa hawakuja kutupa ripoti kamili waliyopeleka kwa rais huyo.

Walituambia wamekubali maelezo yetu na ingekua bora kama tungekuwa tunaeleza zaidi watu wajue na tusiwe wasiri.”

Maelezo hapo juu yanadhihirisha wazi kuwa Freemasons  ni dini ya shetani, ndiyo maana mungu wao anaitwa fundi mkuu  na si Yehova anayetajwa kwenye Biblia na madai kuwa taasisi hiyo si dini ni uongo wa hali ya juu usiohitaji hata udadavuzi wa ziada.

MHARIRI
 Nimeamua kuchapa habari hii kwa undani si kwa faida ya kundi hili, au lingine lolote la kishetani, lengo letu hapa ni kuwapa nafasi wasomaji wetu wenye maswali mengi kuhusu utata na maelezo mengi ya uongo kuhusu  uhalali wa makundi ya kishetani ambayo yanaendesha ibada zake katika mazingira ya ajabu. Huu ni wakati wa mwisho na shetani anajitangaza hadharani akitafuta wafuasi wa kuondoka nao.

Kumbuka,  wakati watumishi wa Mungu wakizunguka huko na huku  kuitangaza habari njema za Injili, shetani naye yuko kazini akitumia chambo cha fedha kuwavua  wale waliokwisha vuliwa.  Makundi haya  ni hatari sana hasa kwa vijana wanaotafuta mafanikio ya haraka, chukua hatua wewe  na wengine pia.
    
           source Mfaraguzi Innocent Kimath

Comments

Popular posts from this blog

THE FRACTURE AND SPLINTING

BEST WAYS TO TAKE BLOOD PRESSURE

KUNA VIUMBE WA AJABU WANAOISHI ANGANI!