UMRI MZURI KWA MWANAMKE KUPATA MTOTO (KUZAA)


Tamaa ya kutaka kufanikiwa maishani imeenea duniani kote. Hali imebadilika sana, jinsia ya kike inataka kujitosheleza kwa kila kitu. Lakini mabadiliko ya kibaiolojia yanabaki vile vile mfano kuzeeka nk.
Mafanikio wanayowaza wengi ni utajiri wa pesa na elimu kubwa. Hii imesababisha wanawake wengi kusoma sana na kufanya kazi kupita kiasi, hata kupuuzia suala la kuzaa mapema.
Wengi wanashtuka ikiwa umri wao ni zaidi ya miaka 30, ndio wanakuwa na tamaa ya kuzaa. Kuchelewa kwao kuzaa kunaweza kuwa kwa taabu ama kuzaa watoto wenye matatizo mengi ya kiafya.
Kwa miaka mingi, wataalamu wengi wa afya ya uzazi bado wanaamini miaka 20-35 ndio umri sahihi kushika mimba na kuzaa.
Pia, wengi wakifikiri matatizo mengi ya uzazi huongezeka baada ya miaka 35 na huwa zaidi baada ya miaka 40.
Kwa wenzi wawili wanaoishi pamoja, kuchelewa kuzaa huathiri pia wenza wa kiume, ambapo mbegu za uzazi za mwanaume hudhorota kila mwaka upitao na watoto wamaotokana na wanaume wazee huwa na hatari zaidi ya kupata matatizo ya akili na matatizo ya chembe za urithi.
KUBALEHE
Kubalehe ni hatua muhimu sana lupotia ili kuweza kuzaa. Wastani wa kubalehe na kuvunja ungo kwa wasichana ni miaka 9-12 kwa sasa, ingawa miaka ya zamani ilikuwa kuanzia miaka 12-14.
Baada ya kubalehe binti anakuwa na uwezo wa kushika mimba, japokuwa uwezekano huongezeka zaidi kati ya miaka 20-30, baada ya hapa uwezekano huanza kupungua.
Kulingana na The American College of Obstricians & Gynecologists uwezo wa wanawake kuzaa hupungua katika umri wa miaka 32 na hupungua kwa kasi zaidi katika umri wa miaka 37.
Uwezo wa wanawake kuzaa hupungua vile umri unaongezeka kwa kuwa wanawake wanapobalehe wanakuwa na idadi kamili ya mayai katika ovari zao. Namba hii hupungua vile mwanamke anavyozeeka. Pia mayai hayazalishwi kiurahisi kwa wanawake wenye umri mkubwa ukilinganisha na mabinti wadogo.
Kulingana na National Institute for Health & Clinical Excellence (NICE) ya Umoja wa madola (UK), kwa wanawake wenye miaka 35, ni wanawake 94 kati ya 100 wanaweza kupata ujauzito wakifanya ngono kwa ukawaida ndani ya miaka 38, ni wanawake 77 kati ya 100 wanaweza kushika ujauzito.
Magonjwa ya njia za uzazi kama Endometriosis na Uterine fibroids yanawatokea zaidi wanawake wenye umri mkubwa ambayo husababisha mwanamke kutoshika mimba.
Wanawake wenye umri zaidi ya miaka 35 wanaoamua kushika ujauzito wanakabili hatari ya kupanda kwa shinikizo la damu. Kupanda kwa shinikizo la damu wakati wa ujauzito huathiri kondo la nyuma (Placenta) ambalo hutoa lishe kwa kijusi (kitoto kilicho tumboni) hali ambayo huathiri moja kwa moja ukuaji wake.
Pia, hatari ya kupata kisukari kwa wanawake wanaoshika ujauzito wakiwa na miaka 35 na zaidi, huongezeka sana. Kisukari kipindi cha ujauzito huongeza hatari ya kutoka mimba (Miscarriage), kuzaa mtoto mwenye kasoro au kuzaa mtoto mkubwa kupita kiasi.
TAFITI YA HIVI KARIBUNI
Jambo la kushtusha, ni matokeo ya utafiti uliofanyika Sweden, watafiti wanadai hatari ya matatizo ya uzazi huanza mapema tu pale mwanamke anapofikisha miaka 30.
Utafiti uliochapishwa kwenye jarida la magonjwa ya uzazi (Journal of Obstetrics & Gynacology) uliofanywa na watafiti kutoka Taasisi ya Karolinska ya nchini Sweden umegundua katika nchi tajiri duniani wanawake huzaa wakiwa na umri mkubwa kitu kinachopelekea kuongezeka kwa hatari ya kuzaa watoto njiti (Preterm birth), ukuaji hafifu wa vichanga na kuzaa watoto wafu (Stillbirth).
Ili kubainisha hatari kati ya makundi tofauti ya umri ya wanawake wanaozaa kwa mara ya kwanza, watafiti walitumia takwimu za vizazi toka hospitali za Sweden na Norway, zilizokusanya taarifa za karibu wanawake milioni moja, kati ya mwaka 1990 na 2010.
Hatari ya kuzaa watoto njiti (Premature birth) na kuzaa watoto wafu huongezeka kuanzia miaka ya 30 ingawa toka zamani, miaka 35 ndio ilitambulika kuwa mwanzo wa hatari kwa wanawake kupata watoto, lakini utafiti huu mpya unataja mwanzo tu wa miaka 30 hatari ya kupata matatizo katika uzazi huanza.
Kwa kulinganisha kati ya kundi la umri wa miaka 25-29 na 30-34, wanawake wa miaka 30-34 wenye mimba za kwanza walikuwa na hatari ya kuzaa watoto njiti kwenye wiki 22-31 za ujauzito au kuzaa watoto wafu.
Kikosi cha watafiti kiligundua pia sababu zingine zinazoweza kuleta matatizo ya uzazi mfano wa sababu hizo ni kama kuvuta sigara au kuwa mnene kuliko kawaida.
Ulla Waldenstrom, profesa wa kitengo cha afya ya wanawake na watoto katika taasisi ya Karolinska alisema : 'Tumeshangazwa na kuongezeka kwa hatari za uzazi katika umri mdogo sana.'
Prof. Waldenstrom aliendelea ; 'Wanawake wanaweza ona hatari ni ndogo ila kwa jamii kiujumla kuna idadi kubwa ya matatizo yasiyo ya lazima kwao wanawake wanaozaa baada tu ya miaka 30. Hivyo nashauri wanawake na wanaume wapewe taarifa mashuleni juu ya umuhimu wa umri katika uzazi.'
Alipoombwa ushauri kwa wanawake wenye umri zaidi ya miaka 30 wanaotaraji kuzaa, Prof. Waldenstrom alisema ; 'Ushauri bora ni kuepuka uvutaji wa tumbaku/sigara na kuepuka unene, kama inawezekana.''
KIPINDI CHA KUKOMA HEDHI (MENOPAUSE)
Wataalamu wa afya wanasema kwamba mwanamke amekoma hedhi anapokosa kupata hedhi kwa miezi 12 mfululizo. Ni wanawake wachache hukoma kupata hedhi ghafula, yaani, wanakosa hedhi mwezi mmoja unakuwa mwisho wa kuipata.
Wanawake wengi huanza kipindi hiki wakiwa na umri wa miaka 40 na kitu, lakini kwa wengine huanza wakiwa wamechelewa wakiwa na miaka 60 na kitu.
Kutokana na mabadiliko ya kiwango cha homoni kinachotokezwa, huenda mwanamke akakosa kupata hedhi pindi kwa pindi, akapata hedhi wakati ambao hakutarajia au akavuja damu nyingi isivyo kawaida wakati wa hedhi. Pia huenda mwanamke akashuka moyo, hisia zake zikabadilikabadilika na hilo linaweza kumfanya alielie bila sababu, na pia asiwe makini sana na asahau mambo.
Kipindi cha kukoma hedhi huwa tofauti kwa kila mwanamke. Dalili zinaweza kuonekana kipindi hicho ni pamoja na joto la ghafula mwilini, ambalo huenda likafuatiwa na kuhisi baridi. Dalili hizo zinaweza kumfanya mtu akose usingizi na kuishiwa na nguvu.
Baadhi ya wanawake hupatwa na joto la ghafla mwilini kwa mwaka mmoja au miaka miwili wakati wa kipindi hicho cha kukoma hedhi.
Wengine hupatwa na hali hiyo kwa miaka mingi na wachache sana husema kwamba wao hupatwa na joto la ghafula mara kwa mara maisha yao yote.
Ni busara mtu afanyiwe uchunguzi wa kiafya kabla ya kuamua kwamba joto la ghafula linasababishwa na kukoma kwa hedhi. Kwa kuwa kuna matatizo mengine ya kiafya yanaweza kuleta joto la ghafula mfano ugonjwa wa dudumio, malaria, homa ya matumbo n.k
JINSI YA KUISHI VIZURI KIPINDI HICHO
Mabadiliko ya mtindo wa maisha yanaweza kupunguza baadhi ya matatizo hayo mfano kuacha kuvuta sigara, kupunguza au hata kuacha kunywa vileo, vinywaji vyenye kafeini na vyakula vyenye sukari au vikolezo ambavyo vinaweza kusababisha joto la ghafula mwilini.
Kufanya mazoezi husaidia sana kupunguza matatizo yanayohusianishwa na kukoma kwa hedhi. Kwa mfano, mazoezi yanaweza kupunguza kukosa usongizi na kusaidia kuboresha hali ya kihisia na pia huimarisha mifipa na afya ya mtu kwa ujumla.
Ili kumsaidia mwanamke kukabiliana vizuri na kipindi hicho cha kukoma kwa hedhi, huenda madaktari wakampa homoni, vitamini na madini, na dawa za kutibu kushuka moyo.
Pia ni jambo la busara kuwaambia uwapendao hali unayokabili ili wakuonyeshe upendo na wakupe msaada unaouhitaji wakati wa hali yako.
Kipindi hicho kinapokwisha, wanawake ambao hutunza afya yao, wanapata tena nguvu na kuendelea kufurahia maisha.
Asanteni sana kwa kufuatana nami.
                          
   

Comments

Popular posts from this blog

THE FRACTURE AND SPLINTING

BEST WAYS TO TAKE BLOOD PRESSURE

KUNA VIUMBE WA AJABU WANAOISHI ANGANI!