Kuvimba Miguu na Vifundo cha Miguu Kipindi cha Ujauzito (Edema).

 

Mwili wa mjamzito unabadilika kwa kasi sana na kumfanya asijisikie vizuri na kukosa utulivu wa mwili na akili. Moja ya mabadiliko ya mwili ambayo wajawazito wengi wanapata wasiwasi nayo kipindi cha ujauzito ni ni miguu na vifundo vya miguu kuvimba. Edema inaathiri karibia robo tatu ya wanawake wajawazito. Mara nyingi inaanza wiki ya 22 mpaka 27, inaweza kubaki hata baada ya kujifungua.

Katika makala hii tutajadili kwanini miguu inavimba kipindi cha ujauzito, lini unaweza kuona hali hii, lini umuone daktari, na vidokezo rahisi vinavyoweza kukusaidia kukabiliana na hali hii.

Nini chanzo cha miguu kuvimba kwa wajawazito?

Miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito

Ongezeko la kasi la viwango vya homoni ya projesteroni hupunguza kasi ya umeng’enyaji wa chakula. Hii inaweza kusababisha kuvimbiwa tumboni, vilevile unaweza ona mikono, miguu au uso wako umevimba kiasi.

Ikiwa utashuhudia mikono, miguu na uso wako kuvimba sana mapema hii, haswa kama uvimbaji huu unaambatana na dalili nyingine kama kizunguzungu, kuumwa kichwa au kutoka damu, ni jambo la hekima kuwasiliana na mkunga au daktari anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako.

Miezi mitatu ya pili ya ujauzito

Kipindi hiki kinaanza na wiki ya 13 ya ujauzito. Ni kawaida kuanza kushuhudia miguu kuvimba kipindi hasa ikiwa una simama mda mrefu au hali ya hewa ya sehemu unayoishi ni joto.

Uvimbe huu unasababishwa na kuongezeka kwa kiasi cha damu na majimaji ndani ya mwili. Kiasi cha damu huongezeka kwa karibia asilimia 50 kipindi cha ujauzito, ukiunganisha na uhifadhi mwingi wa maji ya homoni (hormonal fluid retention).

Maji haya ya ziada yatasaidia kuandaa na kulainisha mwili wako kwaajili ya kujifungua. Punguza wasiwasi maji haya ya ziada yatapungua kwa kasi baada ya kichanga wako kuzaliwa.

Kipindi cha mwisho cha miezi mitatu ya ujauzito

Wajawazito wengi wanapatwa na tatizo hili la miguu kuvimba kipindi hichi, kinachoanza wiki ya 28. Kadiri wiki zinavyosonga mbele na kukaribia wiki ya 40, ndivyo vidole vyako vya miguuni vitakavyozidi kuvimba.

Edema inatokea pale majimaji ya mwili yanapo ongezeka ili kuhakikisha mtoto na mama mjamzito wanaendelea kukua vizuri, majimaji haya yanachukua nafasi katika tishu na kusababisha mwili kuvimba. Ukuaji wa uterasi unasababisha mgandamizo kwenye mishipa ya nyonga na venakava (mshipa mkubwa unaopatikana upande wa kulia unaohusika na kurudisha damu moyoni kutoka miguuni), hali hii inaweza kupunguza kasi ya mzunguko wa damu kutoka kwenye miguu kurudi kwenye moyo (usiwe na wasiwasi, hali hii sio hatari-itakufanya usiwe katika hali ya utulivu tu). Matokeo yake miguu, mikono na vifundo vya miguu kuzidi huvimba.

Sababu nyingine zinachangia miguu kuvimba kipindi hichi ni pamoja na:

  • Hali ya hewa-joto.
  • Kuongezeka uzito kwa kasi.
  • Kukosa mlo kamili.
  • Unywaji wa kahawa na bidhaa zenye kafeini.
  • Kutembea kwa miguu au kusimama mda mrefu.
  • Kutokunywa maji ya kutosha.

Je, kuna hali za hatari zinazohusiana na kuvimba kwa miguu na vifundo vya miguu?

Hata hivyo ikiwa mikono au uso wako ukavimba na kudumu zaidi ya siku bila kupungua (ndani ya usiku mmoja) wasiliana na daktari anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako.

Kuvimba kupita kiasi kunaweza kuwa ishara ya kifafa cha mimba-huwa inaambatana na dalili nyingine kama shinikizo kubwa la damu, kuongezeka uzito kwa kasi na uwepo wa protini katika mkojo. Ikiwa shinikizo na mkojo wako vitaonekana kuwa kawaida (kila miadi unachunguza), hakuna haja ya kupata wasiwasi.

Kuvimba kwa mguu mmoja (mguu wa kulia) ni ishara ya hali inayoweza hatarisha maisha “DVT” (deep vein thrombosis)-inatokea pale damu inapoganda katika mshipa ulio ndani(deep) .Ishara nyingine ni pamoja na uzito au maumivu ya mguu yanayozidi kila ukisimama, ngozi ya mguu inakua nyekundu na moto pale unapoigusa. Ikiwa umeoona ishara hizi wasiliana na mkunga wako mara moja.

Muda mwingi, miguu kuvimba ni ishara nyingine ya kazi nzito mwili wako unafanya kukuza maisha mapya ya mtoto anayekua tumboni. Hata hivyo wakati mwingine miguu kuvimba ni ishara ya hali hatari sana. Moja ya hali hizi ni kifafa cha mimba. Hali hii huanza wakati wa ujauzito na kusababisha shinikizo kubwa la damu ambalo ni hatari.

Muone daktari ikiwa utaona ishara zifuatazo:

  • Kuvimba ghafla kwa miguu,mikono, uso na kuzunguka macho.
  • Kuvimba kupita kiasi.
  • Kizunguzungu au kushindwa kuona vizuri.
  • Maumivu makali ya kichwa
  • Kuchanganyikiwa
  • Shida katika upumuaji.
  • Ikiwa utashuhudia mguu mmoja umevimba, ukiambatana na maumivu, kubadilika rangi na kuwa wa moto.

Jinsi gani ya kukabiliana na kuvimba kwa miguu na vifundo vya miguu.

  • Weka kikomo cha ulaji wa chumvi. Moja ya njia ya kupunguza miguu kuvimba kipindi cha ujauzito ni kuweka kikomo katika ulaji wa vyakula vyenye sodiamu (chumvi). Chumvi inafanya mwili utunze maji ya ziada. Jaribu kuepuka kula vyakula vilivyohifadhiwa kwenye makopo-vina viwango vikubwa vya sodiamu. Epuka pia kuongeza chumvi kwenye chakula mezani. Tumia viungo kama majani ya “rosemary”, giligilani, tangawizi kuongeza ladha kwenye chakula chako.
  • Kunywa maji ya kutosha. Kunywa maji glasi 8 mpaka 10 kwa siku itakusaidia kuondoa sodiamu ya ziada na taka mwili nyingine.
  • Ongeza ulaji wa vyakula vyenye potasiamu. Potasiamu inasaidia mwili kufanya uwiano wa kiasi cha majimaji unayotunza. Virutubisho unavyotumia kipindi cha ujauzito vina potasiamu ya kutosha kwaajii ya mama mjamzito, lakini vilevile ni muhimu kula vyakula vyenye potasiamu ya kutosha. Baadhi ya vyakula vyenye asilia ya kuwa na patasiamu nyingi ni pamoja na: viazi mviringo na maganda yake, viazi vitamu na maganda yake,ndizi, spinachi, maharagwe, juisi za matunda (chungwa, karoti, pasheni, na komamanga), mtindi na samaki aina ya “salmon. 
  • Epuka kukaa au kusimama kwa muda mrefu. Ikiwa unafanya shughuli inayokutaka kusimama kwa muda mrefu, chukua mapumziko mara kwa mara na kaa kitako. Ikiwa unakaa sana, tumia dakika 5 kwa kila saa, kusimama na kutembea kidogo.
  • Tembea. Matembezi ya hata dakika 5 mpaka 10 kwa siku yanaweza kuboresha mzunguko wa damu na kusaidia kupunguza miguu kuvimba. Hii pia ni njia nzuri ya kufanya mazoezi wakati wa ujauzito.
  • Vaa viatu visivyokubana. Viatu vinavyokuacha huru ni muhimu katika kupunguza uvimbe wa miguu, vile vile hukinga matatizo ya mgongo na nyonga yanayoletwa na mabadiliko ya mkao (centre of gravity) na kuongezeka uzito.
  • Ogelea. Hakuna utafiti unaothibitishakuwa mgandamizo wa maji unapunguza kuvimba kwa miguu wakati wa ujauzito, lakini wanawake wengi wanapata kutulizwa wakitumia muda wao kwenye maji. Jaribu kusimama au kuogelea kwenye maji yenye kina kirefu (kama unaweza). Angalau unaweza kusikia mwepesi,mwili kupoa na pia kuupa mwili wako mazoezi. Utagundua pia miguu yako imepungua kuvimba.
  • Pata “massage”.Kwa msaada ya mwenza wako au sehemu maalum zenye kutoa huduma hii. Kukanda miguu kwa kutumia mafuta maalum inasaidia kusambaza majimaji ambayo yanajikusanya miguuni. Ikiwa unakaribia kujifungua, mweza wako ahakikishe anaepuka kusugua sehemu (acupressure points) ambazo zinahusiana na mikazo ya kujirudia ya mfuko wa uzazi (uterine contractions). Ni busara kumpata mtu aliye na ujuzi wa masaji kukusaidia.
  • Lala kwa ubavu wa kushoto. Ulalaji huu unaweza kuboresha mzunguko wa damu, ambayo inaweza kupunguza miguu kuvimba. Kulala kwa ubavu wa kushoto kuna ondoa mgandamizo wa uterasi kwenye mshipa mkubwa wa damu unaorudisha damu kwenye moyo kutoka miguuni.
  • Weka miguu yako juu. Kama inawezekana kila unapokaa kitako hakikisha miguu imeinuliwa juu, unaweza kutumia kiti kingine, kigoda au ndoo kama egemeo.
  • Epuka soksi au taiti zinazobana. Lengo lako ni kuhakikisha dam una majimaji yanasafiri kwa urahisi (soksi zinazoacha alama ya kubanwa kwenye mguu ni ishara kuwa zinabana).
  • Punguza matumizi ya kafeini. Unywaji sana wa kahawa unachukuliwa kama hatari kubwa kwa mtoto. Inaweza pia kusababisha mguu na vifundo vya miguu kuvimba zaidi. Jaribu chai yenye majani ya mitishamba kama mnana, mchaichai, n.k.
  • Vaa nguo zisizobana. Nguo zinazobana hasa kwenye viwiko, kiuno na vifundo vya miguu inaweza kufanya uvimbe kuongezeka zaidi. Kimsingi, inafanya damu isisambae kwa urahisi. Jaribu kuvaa mavasi yanayoachia mwili- madera na magauni mapana yanayoachia mwili huru, suruali pana zisizobana kwenye kiuno na miguuni ikiwa unaishi eneo lenye baridi.

Kumbuka

Miguu kuvimba ni hali ya kawaida sana kipindi cha ujauzito. Uvimbe huu unasabishwa na ongezeko la kiasi cha maji kwenye mwili, vilevile upungufu wa usambazaji wa maji maji haya.

Ikiwa unapata uvimbe wa miguu uliopitiliza ghafla, ni muhimu kuwasiliana na daktari anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako, kwasababu inaweza kuwa ishara ya tatizo lingine kubwa. Lakini miguu kuvimba kidogo ni kawaida.

Unaweza kuepuka kuvimba miguu kila mara kwa kufanya mzoezi mepesi kwa mjamzito kila mara kama vile kutembea, kunywa maji ya kutosha, pumzika na kula mlo kamili.

Comments

Popular posts from this blog

THE FRACTURE AND SPLINTING

BEST WAYS TO TAKE BLOOD PRESSURE

KUNA VIUMBE WA AJABU WANAOISHI ANGANI!